Blogs
 
ARTICLES
Mwajabe Kizigina     Email : kizigina@nifahamishe.com     
Msukosuko wa vyombo vya fedha duniani na madhara yake kwa Tanzania
             
Msukosuko wa hivi karibuni katika masoko ya fedha duniani umesababisha hofu, wasiwasi mkubwa na hali ya kutoaminiana kati ya vyombo vya fedha. Hali hii imesababisha uhaba mkubwa wa mikopo.

Hadi sasa, nchi nyingi za Bara la Afrika, kwa kiasi kikubwa bado hazijakumbwa moja kwa moja na mkasa huu. Hii pengine inatokana na ukweli kwamba, nchi hizi hazina uhusiano mkubwa na mtandao wa masoko ya fedha wa kimataifa.

Pamoja na ukweli kwamba hivi karibuni nchi nyingi za Afrika, ikiwemo Tanzania, zimetekeleza mageuzi katika masoko ya fedha na hivyo kukaribisha taasisi za fedha kutoka nje, vyombo hivi vimekuwa vikifanya kazi chini ya sheria za nchi husika na mahusiano yake na vyombo vya fedha vya nje yamekuwa bado ni katika misingi iliyoidhinishwa na nchi husika.

Kwa ujumla, benki hapa Tanzania zimeendelea kuimarika na zipo katika hali ya usalama, kama inavyodhihirishwa na viashiria vyote vya uimara wa sekta hii muhimu. Mitaji ni ya kutosha na benki zimeendelea kufanya biashara kwa faida. Karadha kati ya mabenki na taasisi nyingine za fedha iko katika hali ya kuridhisha, na riba ya mikopo kati ya benki na benki ni wastani wa asilimia tano tu, kiwango kinachokubalika.

Benki zinaendelea kutoa mikopo kwa wingi katika sekta binafsi, tofauti na hali ilivyo hivi sasa barani Ulaya na Amerika, ambapo mikopo kutoka mabenki hivi sasa imezidi kupungua. Katika kipindi cha mwaka unaoishia Septemba 2008, mikopo ya mabenki kwa sekta binafsi iliongezeka kwa kiwango kikubwa cha asilimia 48. Huu ni ukuaji mkubwa wa mikopo kwa sekta binafsi ambao haujawahi kufikiwa katika kipindi chote cha kurekebisha na kubinafsisha sekta ya fedha hapa nchini tangu mwanzoni mwa miaka ya tisini. Kuendelea huku kwa hali nzuri ya benki zetu wakati huko Ulaya na Amerika benki zinayumba, inachangiwa na ukweli kwamba, mikopo na dhamana kutoka nje bado siyo mingi kwenye benki za hapa nchini.
Kwa upande mwingine, akiba yetu ya fedha za kigeni (foreign exchange reserves) imeendelea kupanda. Katika kipindi cha miezi 18 iliyopita akiba yetu imekuwa katika kiwango cha Dola za Kemarekani bilioni 2.7. Kiwango hiki cha akiba kinatosha kulipia uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa miezi mitano. Hiki ni kiwango cha juu, ikilinganishwa na nchi nyingi za jirani. Zaidi ya hayo, Watanzania wanazo amana katika fedha za kigeni (foreign currency denominated deposits) kwenye benki za biashara hapa nchini zinazofikia Dola za Kimarekani bilioni 1.6. Wakati huo huo, benki nazo zina akiba katika fedha za kigeni (net foreign assets) inayofikia Dola za Kimarekani milioni 600.


Kiwango cha akiba ya fedha za kigeni tuliyonayo ni muhimu katika kuimarisha shilingi yetu na pia imani katika uchumi wa Tanzania. Katika kipindi cha hivi karibuni, shilingi ya Tanzania iliimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na dola ya Marekani kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera ya fedha ya Benki Kuu ya Tanzania. Sera ya Benki ya fedha za kigeni inalenga kuimarisha masoko ya fedha sanjari na misingi ya kiuchumi (economic fundamentals). Kupanda na kushuka kwa thamani ya shilingi kusikoendana na misingi ya uchumi huwapa matatizo waagizaji na wasafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.
Siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya fedha za kigeni ambayo hayaendani na mahitaji ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Sababu zinazojitokeza kuelezea hali hiyo ni wasi wasi kwamba, msukosuko katika masoko ya fedha duniani unaweza kusababisha uhaba wa fedha za kigeni kwa ajili ya kufanya malipo nje ya nchi. Hivyo baadhi ya washiriki katika soko wanahodhi fedha za kigeni ili kujihami kama uhaba wa fedha za kigeni.

Napenda kuwahakikishia wananchi wote kwamba, tunazo fedha za kutosha kwa ajili ya kufanya malipo ya kawaida ya bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi, wala kujilimbikizia fedha nyingi za kigeni kwa kuwa hii ni gharama isiyo ya lazima.
Hata hivyo, kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, itabidi Tanzania ikabiliane na matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na athari za msukosuko wa fedha duniani. Athari hizo zitatokana na vyanzo vifuatavyo:-

Kupungua kwa vipato katika nchi za Magharibi, kunaweza kusababisha kupungua kwa uwezo wa nchi hizo kununua bidhaa na huduma kutoka nchi nyingine, ikiwemo Tanzania. Hii itasababisha bei za mazao yetu tunayouza nje kuteremka.

Kuongezeka kwa matumizi ya serikali z anchi zilizoendelea kwa ajili ya kuyaokoa mabenki yanayoanguka kunaweza kupungu misaada kw anchi masikini.

Kupungua kwa mikopo au kuongezeka kwa gharama za mikopo kutoka nje, kunaweza kusababisha kupungua kwa uwekezaji hapa nchini.

Kupungua kwa vipato katika nchi tajiri kunaweza kupunguza idadi ya watalii.
Hata hivyo, juhudi za kimataifa zinafanywa ili kukabiliana na msukosuko wa fedha duniani, ili kudhibiti kuenea kwa athari zake.

Benno Ndulu
Gavana
BENKI KUU YA TANZANIA


Comments / Maoni
No comment added
Post your Comments / Toa maoni yako
Heading
Comments


                  
My Other articles
JE NI SAWA BABA KUMUOMBA MSAMAHA MWANAE
JIBU KUHUSU CHUO CHA UZOEFU
Je kuzaliwa kwa mtoto kunapunguza mapenzi?
CHUO CHA UZOEFU.
JE NI SAWA KUMRUHUSU MTOTO WAKO KUWA NA BOYFR
Make Your Man Feel Appreciated
Msukosuko wa vyombo vya fedha duniani na madhara yake kwa Tanzania
Dating Your Coworker Or Boss, Is This A Good idea?
Should Tanzania worry about the credit crunch
Five Ways To Successfully Negotiate A Salary

 
Photo Gallery

 Kipindi na maliza mwng primary schl nikiwa na my dream

 Huku si Kujitakia kifo?
Most viewed news