Blogs
 
ARTICLES
Kassim Baruani     Email : kasbaru@nifahamishe.com     
DEMOKRASIA YA KWELI
             
Demokrasia,hasa kwa nchi za Afrika ni neno ambalo kwa miaka mingi sasa limekuwa likipita masikioni mwa watu wengi hali ya kuwa wengi wao hata hawajui maana na uzito halisi wa neno hilo.

Kwa lugha rahisi,na kwa kifupi,neno demokrasia linaweza kutafsiriwa kama aina ya uongozi wa watu kwa ajili ya watu.Uongozi huo hupatikana kwa kufanyika uchaguzi ambao unatakiwa uwe huru na wa haki.

Ninaposema uchaguzi huru na wa haki namaanisha kwamba wananchi waweze kugombea nafasi za uongozi wanazotaka ikiwa wana sifa zinazostahili,wawe na uhuru wa kuongea na wananchi wenzao kuhusu sera na mipango yao pindi watakapopewa dhamana ya kuwaongoza wenzao ikiwa ni pamoja na kuukosoa uongozi uliotangulia bila uwoga wa aina yoyote kwa kueleza ukweli waziwazi kuhusu “uchafu” na “madudu” yaliyofanywa na uongozi huo na jinsi gani wao wataweza kufanya marekebisho na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wenzao pamoja na nchi kwa ujumla.

Wananchi pia wawe huru kuwachagua viongozi wanaowataka bila uwoga wala vitisho au kununuliwa hati zao za kupigia kura kwa kipande cha sabuni,kilo mbili za sukari na upande wa khanga kwasababu hali zao kimaisha ni duni kiasi kwamba hawawezi hata kukumbuka ni lini ilikuwa mara ya mwisho kwao kunywa chai yenye sukari!

Baada ya uchaguzi huru kufanyika,itendeke haki kwa wagombea na wapiga kura kwa matokeo ya uchaguzi huo kutangazwa katika muda unaotakiwa,tena kama yalivyo,bila kufanyiwa marekebisho ya aina yoyote kwani hivyo ndivyo wananchi walivyoamua.

Baada ya hapo wagombea wote,walioshinda na wale walioshindwa katika uchaguzi huo wanatakiwa wayakubali maamuzi ya wananchi waliopiga kura kwa kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo bila vurugu na kuwapongeza wale waliopewa dhamana na wananchi wenzao ya kuwaongoza mpaka pale utakapowadia wakati wa wananchi kuamua tena nani wanaona na wanaamini kwamba anafaa kupewa dhamana hiyo ya uongozi.Pia wagombea hao walioshindwa kwenye uchaguzi wawe tayari kuwasaidia na kushirikiana na wenzao katika kulitumikia,kulijenga na kuliendeleza taifa lao na si kujenga chuki kwa wenzao,kitu ambacho hufanywa na wale waliotaka uongozi si kwa ajili ya maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla bali kwa maslahi yao binafsi.

Pia Katika demokrasia kunatakiwa kuwe na uhuru wa vyombo vya habari na wananchi waweze kuongea na kutoa mawazo na fikra zao bila kuogopa kwamba vyombo hivyo vya habari vitafungiwa,maisha ya wananchi hao yatakuwa hatarini au serikali “itagundua kwamba wao si raia” baada ya kuwa waliwahi kushika nafasi muhimu za uongozi serikalini,kitu ambacho kinasababisha maswali mengi vichwani mwa watu wengi,ikiwa ni pamoja na,Je,ina maana serikali imejaa wajinga kiasi kwamba hawakuweza kutambua kwamba mtu fulani si raia wa Tanzania kwahiyo hafai kupewa madaraka serikalini?

Uchaguzi uliofanyika tarehe 04/11/2008 nchini Marekani na matokeo yake kutangazwa tarehe 05/11/2008,siku moja tu baada ya wananchi kuwa wamepiga kura,unatakiwa uwe mfano kwa dunia nzima,hasa nchi za bara la Afrika,hususani Tanzania.Uchaguzi huo umeionesha dunia nini maana ya demokrasia ya kweli,kwamba kila mtu ana haki ya kuwa kiongozi ikiwa ana sifa zinazostahili,kwamba uongozi si biashara ya watu binafsi,na kwamba viongozi ni wale wanaochaguliwa na wananchi.Kwa wale waliofuatilia,baada tu ya matokeo kutangazwa,Seneta John McCain alimpigia simu mgombea mwenzake Seneta Barack Obama kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa raisi wa 44 wa Marekani.Katika hotuba yake ya kuyakubali matokeo,Seneta John McCain alisema kwamba wananchi wamefanya uamuzi na anaukubali na kuuheshimu uamuzi huo,ikimaanisha kwamba wananchi ndio wenye uwezo na haki ya kuamua nani awe kiongozi wao,na si vinginevyo.Na pia akaahidi kwamba atamsaidia na kushirikiana na raisi mpya aliyechaguliwa na wananchi katika kuliendeleza taifa lao.Tusishangilie tu kwamba mtu mwenye asili ya Afrika amechaguliwa kuwa raisi wa Marekani na kuishia hapo bali tunatakiwa tujifunze kutokana na uchaguzi huo na turekebishe makosa yetu ambayo tumekuwa tukiyafanya kwa miaka mingi sasa.Na tuhakikishe kwamba hatukubali tena kupelekwa pelekwa kama kundi la kondoo.

Uongozi ni dhamana nzito ambayo watu hawatakiwi tu kuivamia “kichwa kichwa”.Uongozi unatakiwa uwe kwa ajili ya watu na nchi kwa ujumla na si kwa ajili ya maslahi binafsi ya wachache kama wafanyavyo wengi katika nchi za Afrika na hasa Tanzania,ambao siwezi kuwaita viongozi kwani wengi wao wameingia madarakani kinyume na misingi ya demokrasia.Naomba wasomaji mnisaidie kuwapatia jina linalowastahili watu hawa wanafiki,ambao ni sawa na chui waliovaa ngozi za kondoo na pia ni maadui wakubwa wa demokrasia.


Comments / Maoni
No comment added
Post your Comments / Toa maoni yako
Heading
Comments


                  
My Other articles
WAZAZI:WALIMU NA MARAFIKI WA KWANZA WA WATOTO
KITENDAWILI
DEMOKRASIA YA KWELI
Safari ya kilomita 1000...

 
Photo Gallery

 Kipindi na maliza mwng primary schl nikiwa na my dream

 Huku si Kujitakia kifo?
Most viewed news