Blogs
 
ARTICLES
Yona Maro     Email : yona_maro@nifahamishe.com     
Tutumie Runinga Kuleta Mapinduzi Katika Utoaji Wa Elimu
             
TUNAZIKUMBUKA enzi za ukoloni, na miaka ya mwanzo baada ya nchi yetu kupata uhuru, wakati redio zilivyokuwa zinatumika mashuleni kuboresha elimu! Kwa mfano, ilikuwa lazima kusikiliza taarifa ya habari kila siku!


Vile vile, kulikuwa na masomo mengine yaliyokuwa yanafundishwa kwa redio peke yake! Wakati ule, runinga hazikuwapo! Kwa bahati nzuri, leo runinga zipo, lakini kwa bahati mbaya, hazitumiki kuboresha elimu mashuleni! Kwa bahati mbaya zaidi, hata redio hazitumiki!


Wataalam wanatuambia kwamba, uwekezaji katika elimu ndiyo wenye faida kubwa kuliko uwekezaji wa aina nyingine zote!


Ukweli huu unajidhihirisha kwenye nchi kama China, Malaysia, HonKong, Japan na India ambazo zimepiga hatua kubwa za maendeleo kwa kuwekeza kwenya elimu, na hasa elimu ya sayansi na tekinolojia, kwa kiwango kikubwa!


Hakuna nchi isiyowekeza kwenya elimu, na wala haiwezekani kwa nchi kuwekeza pato lake lote kwenye elimu! Je, nchi inatakiwa iwekeze kiasi gani cha pato lake kwenye elimu ili ipate maendeleo ya haraka, yakiwemo ya viwanda?


Kama ilivyo hatari kuendesha gari kwa mwendo wa kasi katika barabara mbovu, vivyo hivyo ni hatari kwa elimu kupanuka kwa kasi kubwa katika nchi yenye uchumi duni! Kupanuka kwa elimu ni lazima kuende sambamba na kupanuka kwa ajira! Kwa maana nyingine, kasi ya uwekezaji katika elimu ni lazima iwe na uwiano na kasi ya uwekezaji katika miradi ya uchumi itakayoongeza nafasi za ajira!


Kwa kuwa pato la nchi ni lazima pia litumike kutoa huduma kama za afya, maji na nishati, tunaona kwamba, changamoto iko kwenye uwezo wa kukokotoa asilimia muafaka ya pato la taifa kwa ajili ya kuwekeza kwenye elimu! Isitoshe, kuna changamoto ya kukokotoa asilimia za kuwekeza kwenye ngazi zote za elimu, kama sekondari na elimu ya juu, na asilimia za kuwekeza kwenye masomo ya sayansi, ikilinganishwa na masomo mengine!


Wataalam katika fani ya uhandisi wanatuambia kwamba, ili kuwe na ufanisi wa wahandisi, ni lazima idadi yao katika nchi iwe na uwiano na idadi ya mafundi! Isitoshe, uwiano huo unafahamika kimataifa! Mawazo sanifu yanaonyesha kwamba, ili kuwe na ufanisi katika shughuli zote za maendeleo katika nchi, ni lazima kuwe na uwiano muafaka wa wahitimu wa fani zote! Tunaona kwamba, jukumu la kuratibu elimu katika nchi ni zito, kwa sababu ya umuhimu wa kukokotoa takwimu nyingi na kuwa na mipango itakayokidhi mahitaji!


Katika nchi tajiri zenye uwezo wa kumpa kila mtoto elimu inayoendana na kipaji chake, uwiano kati ya fani mbali mbali unajipanga bila ulazima wa kuingiliwa na wataalam! Tunasema hivyo kwa sababu tunaamini kwamba, Mwenyezi Mungu anapanga vipaji katika nchi kwa ufanisi wa kuhakikisha uwiano huo! Kasheshe iko kwenye nchi maskini zisizokuwa na mifumo ya kutambua na kuendeleza vipaji!


Nchi maskini, kama Tanzania, zina matatizo mengi yanayofanya kazi ya kuratibu elimu kuwa ngumu, yakiwemo uhaba wa shule na vyuo, uhaba wa maabara, uhaba wa walimu, uhaba wa vitabu na hata uhaba wa madawati! Pamoja na kuipongeza wizara ya elimu kwa jitihada zake za kuongeza idadi ya walimu, na pamoja na kuipongeza wizara ya fedha kwa kuipa sekta ya elimu kipaumbele katika bajeti ya mwaka 2007/2008, tunahoji kwamba, jitihada hizi hazitoshelezi mahitaji! Kwa mfano, hata baada ya walimu walio vyuoni kuhitimu, bado kutakuwa na shule zitakazokosa walimu!


Isitoshe, kuna masomo kama Hisabati na Fizikia ambayo yana tabia ya kuwa na walimu wachache katika nchi zote! Kwa bahati nzuri, tekinolojia ya mawasiliano inaweza kutumika kwa ajili ya kupunguza makali ya ukosefu wa walimu! Yaani mwalimu mmoja anaweza kufundisha shule nyingi kwa wakati mmoja!


Mathalan, ni rahisi kununua runinga moja yenye kioo kipana, kwa chini ya shilingi milioni mbili, ikatumika kufundishia masomo mengi, kuliko kuajiri walimu, ambao hawapo, katika kila somo! Yaani bajeti ya kuwalipa mishahara walimu hao ni maradufu ya bajeti ya kununua runinga! Kwa upande wa shule za msingi, tunashauri wizara ya elimu irudishe vipindi vya redio, kwa masomo kadhaa!


Faida za vipindi hivyo ni pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kusikiliza na kuelewa bila kumuona anayezungumza! Ni pamoja na kujenga jamii ya wananchi wenye tabia ya kusikiliza redio! Wanaotembelea sehemu za starehe ni mashahidi kwamba wananchi wengi hawana tabia ya kusikiliza hata taarifa muhimu za redio ama runinga! Pengine wakati umefika wa kutoa angalao mitihani ya mahojiano katika nafasi zote za kazi!


Uamuzi wa aina hii utajenga tabia ya kusoma magazeti, kusikiliza redio na runinga, na kufuatilia matukio muhimu ya kitaifa! Tunahoji kwamba, uraia ni pamoja na kufahamu matukio muhimu ya nchi, na ndiyo maana simba wa Serengeti haitwi raia, licha ya kwamba kazaliwa Tanzania, na anafanya kazi ya kuliingizia taifa fedha za kigeni


Comments / Maoni
No comment added
Post your Comments / Toa maoni yako
Heading
Comments


                  
My Other articles
Je unajua jinsi ya kujilinda unapotembelea tovuti kama Facebook au hi5?
Usiingie kichwa kichwa, Hii ni kwa usalama wako
Tutumie Runinga Kuleta Mapinduzi Katika Utoaji Wa Elimu
Jamii Ijihadhari na Soko Huria
Hakuna Mtetezi wa mapambano ya Wananchi
MAPINDUZI BILA KUMWAGA DAMU

 
Photo Gallery

 Kipindi na maliza mwng primary schl nikiwa na my dream

 Huku si Kujitakia kifo?
Most viewed news