Blogs
 
ARTICLES
Yona Maro     Email : yona_maro@nifahamishe.com     
Hakuna Mtetezi wa mapambano ya Wananchi
             
MNAMO Julai 4, 1776 vuguvugu la kujikomboa kwa Waamerika lilishika kasi ambapo mwanadiplomasia Thomas Jefferson alitoa andiko la uhuru lililonadi kujitoa kwa Amerika kutoka chini ya himaya ya kikoloni ya Mfalme wa kiingereza aliyeitwa George III.

Ilipofika 1783 Wananchi walichachamaa mno maandamano huku na kule utawala ukashinikizwa kukubali matakwa ya wengi. Waingereza walitii shinikizo wakiwa na uwezo mkubwa kijeshi mbali ya kuwa taifa kubwa wakati huo.

Kwanini Waamerika waliamua kujitoa muhanga huku wakijua wazi hatari ya jaribio lao? Ni vipi waliweza kujiamini kwamba walikuwa sahihi katika mgogoro wao na Uingereza? Ni kwa kiasi gani waliweza kuamini kuwa hali ya baada ya kujikomboa ingekuwa bora kuliko kuishi chini ya ukoloni? Haya ni maswali yanayoulizwa na kujibiwa na waandishi wengi wa masuala ya siasa zama hizi.

Msukumo mkubwa wa vuguvugu la kujikomboa ni imani waliyokuwa nayo waamerika zama hizo kwamba matatizo yao yangeweza kutatulika na kwamba wangeweza kupata utatuzi na namna nzuri ya kukabiliana nayo.

La mwanzo waliloanza kama msingi wa yote katika kujiondoa na hali iliyokuwepo ni lile la kuweka muafaka wa kijamii (Katiba) ambao uliwahitaji Wanajamii wote kujifunga, na huo huo kuwa dira ya utendaji wa serikali zilizokuja kuongoza.

Katika mkataba huu serikali ilipewa nguvu fulani lakini ikitii na kufuata sheria na kanuni zilizowekwa na kutumia nguvu hizo kwa ajili ya maslahi ya raia wote. Na pale viongozi wanapozitumia nguvu hizo visivyo au kwenda kinyume na kanuni basi mkataba ule ungekoma mara moja. Raia walipewa uwezo kikatiba kuvunja mkataba na serikali iliyoko madarakani pale inapotenda kinyume na makubaliano.

Akifafanua mkataba huo Bwana Thomas Jefferson alisema: " Ni haki ya raia kuasi au kuiondoa serikali iliyo madarakani na kuweka mpya (muda wa kuwa imekwenda kinyume na kanuni zilizowekwa kikatiba)". Waamerika wamedumu na hali hiyo hadi hii leo wakiheshimu mambo muhimu matatu:

(a) Mamlaka na haki ya kuunda serikali yanatoka kwa wananchi (raia).

(b) Nguvu inazopewa serikali zina ukomo ambao ukikiukwa watu hawapaswi kuendelea kutii.

(c) Wananchi wanayo haki kuiasi na kuiangusha serikali isiyokidhi matakwa yao.

Kutokana na haya, leo hii Amerika haina upuuzi wa kiongozi kufanya atakavyo huku dola ikimpa ulinzi au vyombo vya habari kumjenga. Serikali ni ya watu na wao ndio wenye kibali cha kusema ndio au hapana na maamuzi yao kuheshimiwa kwa mujibu wa katiba. Kura na chaguo la wengi ndio leseni ya uongozi si vinginevyo jamii ya huko iko imara (strong civil society) kulipigania na kulisimamisha hilo.

Bahati mbaya mataifa 'machanga' hasa ya Kiafrika pamoja na kujaribu kuiga mfumo huo wa utawala bado zimeendelea na kasumba ya watu fulani kupewa uwezo na haki isiyowajibika kwa yeyote ambao huburuza wengine kwa kutumia mwanya wa kutodhibitiwa kikatiba.

Nchi yetu hivi sasa inapita katika mkondo ambao kama hawatapatikana watu wenye kujali na kutafakari mustakbali wa jamii, iko hatari kubwa mbeleni. Zipo dalili za wazi zinazoashiria mapigano mabaya ya wenyewe kwa wenyewe. Umaskini na ulafi huenda vikawa vyanzo vikuu. Ukaidi na kutowajibika zikawa chagizo. Chuki, upendeleo, ukandamizaji na dhulma kuwa pambio za mtafaruku huo wa kijamii.

Lakini msingi wa mapungufu hayo ni ukweli kwamba nchi yetu haijawa na muafaka makini wa kijamii. Na zimekuwepo jitihada za makusudi kudumisha hali hiyo! Suala la white paper ni ushahidi mmojawapo!

Kinyume na hali tuliyoileza mwanzo kule Amerika, hapa kwetu tokea taifa 'liundwe' wananchi hawajapata fursa ya kukutana kimakundi, kabila, dini na kadhalika kujadili namna watakavyoishi wakizingatia tofauti walizonazo huku wakisheshimiana kama raia wa nchi moja.

Hali hiyo imetoa fursa kwa watendaji hasa wa vyombo vikuu vinavyounda dola kuifikisha nchi hapa ilipofikia. Hatari kubwa inayonyemelea nchi yetu, ni kwamba wananchi wamechoka na hali hiyo.

Malalamiko yaliyozagaa mijini juu ya hali ngumu ya maisha inayotokana na vipato duni na serikali kushindwa kuboresha huduma mbali mbali, miundo mbinu mibovu, viongozi kuahidi na kusema uongo na kadhalika; rushwa na upendeleo katika vyombo vya sheria na Bunge kuwa mali ya vyama badala ya kujadili mambo ya wananchi, ni ushahidi kwamba jamii yetu, inakanyaga mahali penye mlipuko.

Ni hakika alivyosema kiongozi mmoja mstaafu wa jeshi kwamba duniani kote wananchi ni jeshi hatari linaloweza kuisambaratisha nchi iliyostawi. Ni jeshi baya kuliko lile lenye mafunzo maalum na vifaa bora kambini.

Ni busara kubwa kama tungeanza kufikiria mkondo wa historia yetu. Tanzania isifikie mahali wananchi wakaamua kusema basi lolote na liwe, hapatakuwa na kiongozi, raia wa kawaida, mwanajeshi au polisi wa kuweza kuhimili mikiki yake! Nchi itasambaratika kufumba na kufumbua.

--
Yona Fares Maro


Comments / Maoni
No comment added
Post your Comments / Toa maoni yako
Heading
Comments


                  
My Other articles
Je unajua jinsi ya kujilinda unapotembelea tovuti kama Facebook au hi5?
Usiingie kichwa kichwa, Hii ni kwa usalama wako
Tutumie Runinga Kuleta Mapinduzi Katika Utoaji Wa Elimu
Jamii Ijihadhari na Soko Huria
Hakuna Mtetezi wa mapambano ya Wananchi
MAPINDUZI BILA KUMWAGA DAMU

 
Photo Gallery

 Kipindi na maliza mwng primary schl nikiwa na my dream

 Huku si Kujitakia kifo?
Most viewed news