Blogs
 
ARTICLES
Kassim Baruani     Email : kasbaru@nifahamishe.com     
KITENDAWILI
             
Kwa muda mrefu nilikuwa nikijiuliza swali ambalo lilikuwa likiniumiza sana kichwa bila mafanikio yoyote katika kulipatia jibu sahihi.Baada ya kuumia kichwa kwa muda mrefu nikaamua niache kujishughulisha na swali hilo.

Baada ya muda si mrefu tokea nidhani kwamba kichwa changu kimepumzika ,swali nililojaribu kulikwepa limerudi tena kwa kishindo na kunisababishia maumivu makali zaidi ya yale niliyokuwa nikiyapata siku za nyuma.
Maumivu haya yanatokana na mchanganyiko wa hisia tofauti zitokanazo na ushindi wa Barack Obama katika uchaguzi uliofanyika Marekani mwezi mmoja uliopita.

Kwa upande mmoja ninajumuika na watu wengine wa dunia nzima nikiwa na furaha kutokana na tukio zima.Zaidi najumuika na waafrika wenzangu na wale wote wenye asili ya Afrika katika kufurahia mafanikio ya Barack Obama,akiwa kama mtu mwenye asili ya Afrika,kitu kinachoonesha kwamba mtu yeyote anaweza kufanikiwa katika jambo lolote endapo atafanya juhudi ya kutosha,bila kujali rangi ya ngozi au asili ya mtu huyo.
Hili linaonekana wazi kwani wapo watu wengi wenye asili ya Afrika walioweza kupata mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwa viongozi wazuri.

Kwa upande mwingine mafanikio hayo ya Barack Obama yamenipa uchungu sana hasa pale ninapoifikiria hali ya nyumbani,Afrika,hususani Tanzania,na ninazidi kujiuliza tena na tena,tatizo hasa ni nini?Kuna wakati nilikuwa nikifikiri kwamba labda tatizo halisi lipo katika elimu tunayopatiwa Afrika,-hili lina ukweli fulani ndani yake.Lakini narudi tena kujiuliza;mbona viongozi wengi wa nchi za Afrika wamesoma katika nchi mbalimbali za Ulaya na Amerika,huku wakiona viongozi wa nchi hizo wanavyofanya kazi kwa bidii katika kuzitumikia na kuziendeleza nchi zao halafu bado warudipo nyumbani Afrika wanafanya mambo ya ajabu ikiwa ni pamoja na ufisadi?Kama vile hilo halitoshi,viongozi hao wanasafiri mara kwa mara kwenda Ulaya,Amerika na nchi nyingine wakitumia pesa za wananchi ambao wengi wao ni walala hoi,kiasi cha kufikia kuonekana kama vile huko Ulaya na Amerika pia ni nyumbani kwao!Isingekuwa tatizo endapo safari zao hizo zingekuwa na manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla,badala ya viongozi hao kwenda kusaini mikataba ya ajabu ajabu ambayo wananchi wanafichwa,hawaelezwi inahusu nini ingawa wana haki ya kujua.

Kitendawili hiki hakiwahusu viongozi peke yao,kinawahusu pia wahandisi,madaktari,wahasibu na wengineo katika nyanja tofauti tofauti.
Tukiangalia tutaona kwamba kuna wahandisi wengi waafrika au wenye asili ya Afrika waliosoma Ulaya,Amerika,Japan,China, na katika nchi nyingine zilizoendelea na baada ya hapo wakaweza kuwa wahandisi wazuri na wanafanya mambo makubwa na yenye mafanikio katika nchi hizo ambayo yanachangia katika kuendelea kwa nchi hizo.Kitu kinachoshangaza ni kwamba wahandisi wetu,waliosoma nyumbani na waliosoma katika nchi nyingine wanaporudi nyumbani,wengi wao huingia katika mkondo wa ufisadi na kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili ya kazi zao.Kwa mfano,inakuwaje wahandisi wetu wanapopewa kazi ya kutengeneza barabara huchukua muda mrefu zaidi,na viwango vya barabara hizo vinakuwa vibovu,kitu kinachopelekea barabara hizo kutodumu kwa muda mrefu wakati kazi hiyo hiyo wakipewa wajapani au wachina ambao ndio waliowafundisha baadhi ya wahandisi wetu,huifanya kazi hiyo kwa ufanisi na barabara hizo hudumu kwa muda mrefu?

Madaktari wa kiafrika wanaofanya kazi kwenye nchi zilizoendelea pia hufanya kazi zao kwa bidii,ufanisi na kwa kufuata maadili ya kazi zao.Kwanini nyumbani hali iwe tofauti?Kila siku tunasikia vituko vinavyofanywa na madaktari na wauguzi katika hospitali mbalimbali Tanzania,kwanini?
Mifano ipo mingi ambayo inabidi tuifikirie na tujiulize tena,kwanini?

Kwa kifupi,ukweli ni kwamba mambo yataendelea kuwa yale yale kila siku mpaka hapo tutakapokitegua kitendawili hiki ili tuweze kufanya mabadiliko,mabadiliko ambayo hayatafanywa na mtu mwingine isipokuwa sisi wenyewe.


Comments / Maoni
No comment added
Post your Comments / Toa maoni yako
Heading
Comments


                  
My Other articles
WAZAZI:WALIMU NA MARAFIKI WA KWANZA WA WATOTO
KITENDAWILI
DEMOKRASIA YA KWELI
Safari ya kilomita 1000...

 
Photo Gallery

 Kipindi na maliza mwng primary schl nikiwa na my dream

 Huku si Kujitakia kifo?
Most viewed news